focusmedia Search This Blog

Sunday, February 19, 2017

WAZIRI MKUU AKERWA MBOLEA YA MINJINGU KUPEWA LEBO YA KENYA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema haridhiki na hali aliyoikuta kwenye kiwanda cha kutengeneza mbolea cha Minjingu baada ya kubaini kuwa wanatumia mifuko yenye lebo ya Kenya wakati mbolea hiyo inazalishwa hapa nchini. 

Kutokana na hilo, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa kiwanda hicho waandike barua kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kabla hajamaliza ziara yake Jumatano, Februari 22, 2017 apate nakala ya barua hiyo.

Ametoa agizo hilo (Jumapili, Februari 19, 2017) baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo wilaya Babati akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara. Waziri Mkuu amerejea Babati leo akitokea Dar es Salaam ambako alikuwa na ratiba za kitaifa. 

“Nilikuja kukagua kiwanda baada ya kupokea malalamiko kuwa mbolea hii haikubaliki huko vijijini. Watafiti wameonyesha kuwa ikitumika inasaidia kutoa mazao mengi. Lakini wakati niko kiwandani nimekerwa kukuta mifuko ya kupakia mbolea hii ina anuani ya Nairobi, Kenya wakati mali ghafi inatoka Tanzania,” amesema.

“Ni kwa nini mifuko hii ina anuani ya Kenya? Hapa tulipaswa tuone anuani ya Babati! Je mlipata kibali kutoka serikalini? Tena kuna lebo ya TBS. Kwa nini Tanzania haionekani? Kwani malighafi iko Kenya? Haiwezekani, ni lazima uandike barua na uombe radhi kwa Mheshimiwa Rais Magufuli. Yeye anahimiza ujenzi wa viwanda ndani ya nchi, halafu ninyi mnafanya hivyo?” 

Akiwa ndani ya kiwanda hicho, Waziri Mkuu alikuta baadhi ya mifuko ya mbolea ikiwa imeandikwa: ‘County Government of Bungoma’, ina nembo ya Serikali ya Kenya, na anuani ikionesha kuwa mbolea hiyo imetengenezwa na kiwanda cha mbolea cha Minjingu lakini anuani inasomeka P. O Box 2941 – 00200 Nairobi, Kenbro Industrial Park, Mombasa Road; namba ya simu +254-20-6000-970 lakini mifuko hiyo pia ina muhuri wa TBS.

Baadhi ya mifuko ilikuwa ikipakiwa ndani ya lori tayari kwa kusafirishwa kwenda kwa wateja. Pia amesema atamwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage aje hapa na wanasheria wake na wataalamu kutoka Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC) ili waje kuangalia hatua gani zinapaswa kuchukuliwa. “Kwa staili hii hii tumeona watu wakinunua kahawa yetu na kwenda kuipakia upya huku wakiweka lebo za kwao. Leo hii hata Tanzanite pia inasemwa imetengenzwa India. Hatuwezi kukubali hali hii iendelee,” amesisitiza.

“Tukiruhusu hali hii, watu watajuaje kuwa mbolea hii ambayo ni first class duniani kuwa inapatikana Tanzania? Kiwanda chetu, ardhi yetu, suala la kutangaza nchi yetu kwa kutumia bidhaa zetu litafanikiwa kwa njia hii kweli?”

“Nataka wakati namaliza ziara nipate taarifa ya hili jambo pamoja na nakala ya barua ambayo imetumwa kwa Mheshimiwa Rais,” amesisitiza. 

Akitoa maelezo kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bw. Tosky Hans alimweleza Waziri Mkuu kwamba wametumia lebo hiyo kutokana na makubaliano na wanunuzi jibu ambalo Waziri Mkuu hakulikubali na kusisitiza kuwa anapaswa aombe radhi. Waziri Mkuu kesho anaendelea na ziara yake wilayani Mbulu ambako atatembelea hospitali ya Haydom, kuzungumza na watumishi wa wilaya hiyo na kuzindua shule ya sekondari Singland.
Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa akikagua mgodi wa kiwanda cha mbolea cha  Minjingu wakati alipotembelea kiwanda hicho mkoani Manyara, Februari 19, 2017.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda cha mbolea cha Minjingu mkoani Manyara, Februari 19, 2017


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda cha mbolea cha Minjingu mkoani Manyara, Februari 19, 2017 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza kabala ya kutembelea kiwanda cha mbolea cha Minjingu mkoani Manyara kuanza awamu ya pili ya ziara yake mkoani humo Februari 19, 2017. Kulia ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi, Dkt, Charles Tizeba na kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa ManyaraDkt. Joel Bendera. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Babati, Raymound Mushi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Saturday, February 18, 2017

TANZANIA INA WATUMIAJI WA INTANETI TAKRIBANI MILIONI 20

 TCRA inatueleza kuwa hadi Disemba 2016 tulikuwa na watumiaji wa mtandao wa Intaneti takribani milioni 20.Taifa limejipanga vipi kukabiliana na Vita ya kimtandao na taarifa sahihi kwa manufaa ya kizazi kijacho?

Friday, February 17, 2017

WABUNGE NA WAWAKILISHI WAONYESHA USHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA MAENDELEO YA JAMII NCHINI TANZANIA, MATOKEO CHANYA+ IMEIBUKA NA NEEMA MGAYA MBUNGE WA VITI MAALUMU CCM

MBUNGE VITI MAALUM NEEMA MGAYA ameaazisha kampeni ya kugawa vitabu katika Shule zote za Sekondari mkoani Njombe zaidi ya 80.Hadi sasa amekwisha kugawa Vitabu vya "Kiada na Ziada”katika shule za Sekondari 37 Mkoani humo








Monday, February 6, 2017

MAKAMU WA RAIS AHUDHURIA MKUTANO WA UMOJA WA MATAIFA WA KUWAWEZESHA WANAWAKE KIUCHUMI MJINI DUBAI


Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amehudhuria mkutano wa Jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi kama mmoja wa wajumbe wa jopo hilo. 
Tanzania kama nchi mwanachama ilipata fursa ya kutoa uzoefu wake jinsi Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwawezesha wanawake hususani wale walio katika sekta isiyo rasmi; hasa wakulima na wafanyabiashara wadogo wadogo wanawake ili kuhakikisha wanafaidika na mifumo ya kifedha na kijiditali kama vile kupata mikopo ya gharama nafuu; kuingizwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na huduma zingine. 
Makamu wa Rais alisema pamoja na kila bara kuwa na changamoto zake, bado kuna umuhimu wa dunia kuhakikisha inaweka misingi madhubuti ya  kuinua wanawake kiuchumi hasa kwa wanawake wa ngazi za chini ambao wengi wao wanaishii vijijini.
Alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni  pamoja na mifumo ya sheria na sera zilizopo kuwa bado zinawanyima wanawake haki ya kurithi na kumiliki ardhi hata kama haki hizo zimewekwa kisheria.
Mkutano huo ulileta washiriki takriban 45 kutoka sekta mbalimbali ikiwemo serikali, Taasisi binafsi, wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kumwezesha mwanamke kiuchumi kutoka Jumuiya ya Kimataifa.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akifuatilia kwa makini kwenye mkutano wa Kuwezesha wanawake kiuchumi ambapo wajumbe wa Jopo maalum walikutanna mjini Dubai kujadili Ripoti ya awali ya Jopo hilo

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mrithi wa Mtawala wa Dubai Sheikh Hamdan Bin Mohamed bin Rashid Al Maktoum pamoja na wajumbe wa Jopo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jopo la Umoja wa Mtaifa la Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi ulioanza tarehe 6 februari mjini Dubai.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Siriel Shaidi Mchembe kwenye mkutano wa Kuwezesha wanawake kiuchumi ambapo wajumbe wa Jopo maalum walikutanna mjini Dubai kujadili Ripoti ya awali ya Jopo hilo.

AMIRI JESHI MKUU NA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AMUAPISHA MKUU WA MAJESHI YA ULINZI YA TANZANIA (CDF) PAMOJA NA VIONGOZI WENGINE IKULU JIJINI DAR ES SALAAM


Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Ikulu jijini Dar es Salaam


Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Luteni Jenerali James Mwakibolwa kuwa mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Ikulu jijini Dar es Salaam.


Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Kamishna Jenerali Juma Malewa kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Luteni Jenerali Paul Meela kuwa Balozi nchini DRC Congo, Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi Samuel Shelukindo kuwa Balozi nchini Ufaransa, Ikulu jijini Dar es Salaam.


Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza masuala mbalimbali mara baada ya kumuapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, viongozi wengine wa Jeshi pamoja na Mabalozi Ikulu jijini Dar es Salaam.