Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza katika matembezi hayo katika viwanja vya Green Ground, Oysterbay Jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ya awamu ya Tano imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika sekta ya Afya ikiwemo kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto kwa kuongeza idadi ya wataalamu wa Afya na kuimarisha miundombinu pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kote nchini.
Amesisitiza kuwa ili kuhakikisha huduma za Afya zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa na ubora unaotakiwa Serikali itaendelea kusimamia uwajibikaji kwa watumishi na watoa huduma za Afya mpango utaenda pamoja na kuongeza vitanda kwenye wodi za wazazi na utoaji wa huduma ya Afya bure kwa makundi maalum.
Makamu wa Rais pia amehimiza wadau wa sekta binafsi waendelee kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi nchini ili kufikia malengo ya kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametumia sehemu ya hotuba yake kwa kulipongeza Shirika la AMREF Health Africa Tanzania kwa mipango yake ya kusaidia jamii ya Kitanzania kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo ukiwemo mpango wa kugharamia masomo kwa njia ya ufadhili kwa wanafunzi wanaotoka kwenye familia duni kwa lengo la kuwawezesha kusomea cheti ya uuguzi ukunga.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa mipango na mikakati ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuhakikisha vifo vya wanawake wajawazito na watoto nchini vinapunguzwa kwa kiwango kikubwa kutokana na Serikali kuendelea kutenga bajeti ya kutosha kwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kununua vifaa tiba na kuongeza idadi ya wataalamu.
No comments:
Post a Comment