BENKI ya NMB (National Microfinance Bank Plc) imetangaza gawio la shilingi 104 kwa kila hisa. Wanahisa wa NMB walipitisha kiasi kilichokuwa kimependekezwa katika mkutano mkuu wa Mwaka uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Jumla ya gawio lote litakalolipwa kwa wana hisa ni shilingi Bilioni 52 kiwango ambacho kinaendana na sera ya benki ya kutoa moja ya tatu (33.3%) ya faida baada ya kodi. Benki ilipata faida ya shilingi Bilioni 153.8 kwa mwaka ulioishia disemba 31, 2016; ikiwa ni ongezeko la 2.3% kutoka shilingi Bilioni 150.3 iliyopatikana mwaka uliotangulia.
Ukitoa faida iliyopatikana, NMB iliandikisha mafanikio mbalimbali kwa mwaka 2016. Uzinduzi wa akaunti ya Pamoja ya Wajibu, kuongezeka kwa mawakala zaidi ya 1000 wa NMB Wakala na kuunganishwa kwa halmashauri zaidi ya 150 katika mfumo wa malipo kwa njia za kielektroniki viliongeza upatikanaji wa huduma za kibenki kwa watanzania wengi zaidi ambao awali hawakuwa na huduma hizo, hususani kupitia njia za kielektroniki na hivyo kuongeza hazina ya fedha kwenye benki.
Kutambuliwa kwa NMB na mashirika ya kimataifa kama Moody kuwa na Kiwango cha juu cha ufanisi yaani Stable B1 credit rating inadhihirisha imani waliyonayo wawekezaji wa kimataifa kwa NMB. Wawekezaji wa ndani pia walionyesha Imani yao kubwa kwa NMB kwa kupita Kiwango kilichowekwa na NMB katika uuzwaji wa hati fungani za benki (NMB Retail Bond).
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya NMB – Prof Joseph Semboja, alisema kuwa bodi ya wakurugenzi imeazimia kuweka ulingano kwa kuhakikisha wanahisa wanapata gawio zuri huku benki ikiendelea kuongeza uwekezaji kwenye biashara yake ili kusaidia mipango ya ukuaji wa benki.
“NMB kwa miaka mingi imekuwa ikihakikisha ina mtaji wa kutosha na tunaazimia kuendeleza kasumba hii. Kufikia malengo haya, ni muhimu kufanya maamuzi sahihi hususani tukilenga kuendana na matakwa ya mabadiriko ya kisera hasa matakwa ya mitaji.” Alisema Prof Semboja
Uwiano wa Mitaji wa mabenki nchini unategemewa kubadirika karibuni na hii ni kutokana na matakwa ya benki kuu yanayoyataka mabenki yote ya kibiashara kukubali kuendana na matakwa ya Basel II na matakwa ya kimataifa ya kimahesabu kwa hasara za mikopo za mabenki. Katika muda mfupi, hili litaleta msukumo kwa viwango vya faida ambazo mabenki nchini yatapata.
“NMB imedhamiria kuendelea kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi, pia hivi sasa ambapo mambo mbalimbali yanabadirika. Tunapenda kuwahakikishia ukuaji wa faida utakaotuwezesha kuendeleza ukuaji wa mtaji na kuendelea kuwa benki namba moja nchini,” alisema Mkurugenzi wa NMB – Ineke Bussemaker.
No comments:
Post a Comment