Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia
Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa wilaya ya Serengeti na wa mkoa Mara
kukamilisha haraka awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo ili
kuondoa adha ya wananchi kusafiri kwenda mikoa ya jirani ya Arusha na Mwanza
kwenda kupata huduma afya.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo 6-June-2017 kwenye mkutano wa hadhara mjini
Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara mara baada ya kutembelea ujenzi wa
hospitali hiyo ya wilaya na kuweka jiwe
la msingi.
Makamu wa Rais amesema kutokana na wilaya ya Serengeti
kupata wegeni wengi kutoka nje ya nchi ambao wanaenda kutembelea Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti hivyo ni muhimu kwa
viongozi wa wilaya na mkoa kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo kukamilisha
ujenzi huo haraka ili wananchi waweze kupata huduma za afya za uhakika katika
wilaya yao.
Makamu wa Rais amesema kukamilika kwa ujenzi huo wa awamu ya
kwanza kutaondoa taabu kubwa wanayopata wananchi wa wilaya ya Serengeti katika
kupata huduma ya afya karibu na maeneo yao.
Katika kuunga mkono jitihada hizo za ujenzi wa hospitali ya
wilaya ya Serengeti, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ameahidi kuchangia
kiasi cha shilingi milioni Tano na amewaahidi wananchi wa wilaya ya Serengeti
kuwa atakikisha fedha kutoka Serikalini ambazo zinatakiwa kupelekwa wilayani
humo zinapelekwa haraka ili kukamilisha ujenzi huo.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia amewataka
wananchi kote nchini kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na rushwa
na ufisadi ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na manufaa kwa
wananchi wote.
Amewaomba wananchi nchini wasirudi nyuma katika mapambano
dhidi ya rushwa bali waendelee kubaini watu wanaofanya vitendo hivyo ili
Serikali iweze kuwachukulia hatua kali za kisheria .
Kuhusu tatizo la mimba mkoani Mara, Makamu wa Rais
ameonyesha kuchukizwa na vitendo hivyo na kuomba vyombo vya dola na wananchi
kwa ujumla kushirikiana katika kukomesha mimba za utotoni mkoani Mara.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Mara Dkt Charles Mlingwa
amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa maelekezo yote anayoyatoa katika ziara yake
yatafanyiwa kazi ipasavyo ili kuondoa kero na changamoto zinazowakabili
wananchi.
Mkuu huyo wa mkoa wa Mara ameomba wananchi wa Mkoa wa Mara
kuwepa pembeni tofauti zao za kisiasa bali washirikiane na Serikali katika
utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan bado anaendelea na
ziara yake ya kikazi mkoani Mara ambapo hapo kesho atafanya ziara katika wilaya
za Butiama na Musoma mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment